top of page

Sando International Yasistiza Lishe Bora na Usalama wa Chakula; Wadau Wabomoa Dhana Potofu Kuhusu Ufugaji wa Kuku”

  • Sep 6, 2025
  • 1 min read

Mkurugenzi wa kampuni ya @sando_international amezungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa wadau wa sekta ya kilimo na ufugaji uliofanyika jijini Dar es Salaam. Katika hotuba yake, alisisitiza umuhimu wa kuwekeza kwenye lishe bora ya mifugo na uzalishaji wa vyakula salama visivyo na madhara kwa afya ya walaji, akibainisha kuwa changamoto kubwa katika sekta hii mara nyingi hutokana na taarifa zisizo sahihi na mitazamo finyu inayozuia maendeleo ya wakulima na wafugaji wadogo.

Mkurugenzi huyo alieleza kuwa Sando International imejipanga kuhakikisha kuwa kila mfugaji anapata suluhisho sahihi la lishe, kupitia bidhaa zenye viwango vya kimataifa ambazo zinaleta tija kiuchumi, afya bora ya mifugo, na uhakika wa usalama wa chakula kwa jamii.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wazalishaji wa Vyakula vya Mifugo, Sufian Kyarua, alifafanua kwa kina kuhusu dhana potofu inayosambaa miongoni mwa jamii kwamba kuku wanakuzwa kwa kutumia dawa zenye madhara. Alieleza kuwa madai hayo hayana msingi wa kisayansi, akisisitiza kuwa kinachotumika ni sayansi ya kisasa ya ufugaji pamoja na virutubisho maalum vya lishe, ambavyo husaidia kuku na mifugo mingine kukua kwa njia salama, yenye tija na bila madhara kwa afya ya binadamu.

Aidha, aliongeza kuwa elimu kwa jamii ni jambo muhimu, kwani mara nyingi walaji hukumbwa na hofu kutokana na taarifa zisizo sahihi. Kwa ushirikiano kati ya sekta binafsi, serikali na wadau wa ufugaji, elimu endelevu inaweza kusaidia kuondoa mitazamo potofu na kuhamasisha matumizi ya teknolojia na lishe bora ili kuhakikisha sekta ya mifugo inakuwa nguzo ya uchumi wa Taifa.

Comments


bottom of page